
BENCHIKHA Abdelhak, kocha mkuu Simba kufuatia kufungashiwa virago kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, amefunguka mazito kuhusu sababu ambazo zimepelekea waondoshwe kwenye mashindano.
Benchikha amesema hayo muda mfupi baada ya timu hiyo kurejea nchini wakitokea Misri, huku akiweka wazi kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Al Ahly iliwaongezea ugumu mechi ya marudiano na ndio maana wametolewa.
Kocha Benchikha pia amesema Al Ahly ni timu bora na ina wachezaji wenye uzoefu ambao wanaweza kubadili mchezo muda wowote jambo ambalo pia limechangia kuwagharimu.
Benchikha ambaye amejiunga na Simba msimu huu kutokea ndani ya kikosi cha USM Alger ya Algeria ameongeza kuwa mchezo wa kwanza walipoteza nafasi nyingi za wazi, ambazo zingewaongezea hali ya kujiamini kama wangepata matokeo ya ushindi, lakini hawakuzitumia, huku Al Ahly wenyewe wakipata moja pekee na wameitumia hiyo hiyo.
Licha ya matokeo hayo, kocha Benchikha ametamba kuwa anaamini msimu ujao wakishiriki michuano hiyo watakuwa bora zaidi kwakuwa watakuwa wamejifunza mengi.
“Nafikiri tulipopoteza mechi ya kwanza nyumbani ndipo tulipoongeza ugumu wa mechi ya marudiano, Al Ahly ni timu bora na ina wachezaji wenye uzoefu wa michuano hii.
“Tumejifunza na naamini tutakuwa bora katika michuano hii mwakani kama tukipata nafasi ya kushiriki,” amesema Benchikha.
AHMED: HATUJILAUMU, TUMEJIFUNZA

Kwa upande wa Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema hawajilaumu kwa kutolewa na Al Ahly katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, bali wamejifunza ili wakati mwingine wakishiriki wawe bora zaidi.
Ahmed amesema Al Ahly ndio Mabingwa watetezi wa michuano hii, ndio timu ya Karne ya Afrika na pia kinara wa kuchukua mara nyingi taji hili kwahiyo kutolewa nao sio jambo la kusema watakaa na kuanza kujilaumu.
Ahmed ameongeza kuwa katika miaka sita ambayo wameingia mara tano robo fainali sehemu kubwa ya timu ambazo walicheza dhidi yao zimepotea, lakini Simba imeendelea kubaki palepale na sasa muda umefika wa kusonga mbele.
“Tulianza kucheza na TP Mazembe wakapotea mpaka sasa ndio wanarejea, tukacheza na Kaizer Chiefs wao wamepotea, ikaja Orlando Pirates nao wamepotea na msimu uliopita Wydad Casablanca ambao msimu huu wameishia hatua ya makundi lakini Simba iko vilevile kwahiyo sio jambo jepesi,” amesema Ahmed.
Ahmed ameongeza kuwa baada ya kurejea nyumbani sasa wanaelekeza nguvu katika michuano ya Ligi pamoja na CRDB Bank Federation Cup.
SIMBA YATUA KIGOMA KUWAVAA MASHUJAA

Baada ya kumalizana na kampeni ya mshindano ya kimataifa Simba ambao waliwahi kulelewa na udhamini wa kampuni ya SportPesa sasa wanarejea kwenye mashindano ya ndani ambapo watavaana na Mashujaa FC, kabla ya kuwafuata Singida Black Stars.
“Kikosi tayari kimewasili Kigoma kwa ajili ya mchezo wetu wa hatua ya 16 bora dhidi ya Mashujaa FC utakaopigwa Jumanne ya Aprili 9, mwaka huu saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika na baadae tutaelekea Singida kucheza na Singida Black Stars,” amesema Ahmed.
HAKUNA KULALA, MAPEMA TU KAMBINI

Mara tu, baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Al Ahly kikosi cha Simba chini ya kocha Benchikha kilianza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kutoka Misri ambapo waliwasili na moja kwa moja kikosi kikaingia kambini kuanza maandalizi ya mchezo wa hatua ya 16 bora ya CRDB Bank Federation Cup dhidi ya Mashujaa FC.
Mchezo dhidi ya Mashujaa utapigwa Jumanne ya Aprili 9 saa 10 jioni katika Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma ambapo Simba inahitaji matokeo ya ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali.
Uongozi wa Simba ulisema unajua Mashujaa wapo kwenye kiwango bora na wana timu imara, hasa wakiwa Uwanja wao wa nyumbani, lakini wamejiandaa kuhakikisha wanashinda ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kurudisha kombe hilo mikononi mwao kwani kwa kipindi cha misimu miwili mfululizo ni watani zao wa jadi Yanga ndio wamekuwa wakishikilia
Kwenye misimu hiyo miwili kwa nyakati tofauti Simba bila Benchikha iliambulia kumaliza kwenye hatua ya nusu fainali, wakianza kutolewa na Yanga kwa bao kali la Fei Toto, kabla ya msimu uliopita kuondoshwa na Azam FC kwa kipigo cha mabao 2-1.
