- Gamondi afungukia ishu ya bao la Yanga kimataifa dhidi ya Mamelodi ugenini lililofungwa dakika ya 57
- Kazi kubwa kufanyika kujipanga kwa ajili ya wakati ujao kufanya vizuri zaidi na zaidi
- Ujumbe mzito watumwa kwa watani zao wa jadi Simba suala la robo fainali

YANGA wameweka wazi kuwa wanasahau yote yaliyopita ikiwa ni pamoja na bao la Aziz KI lililofungwa dhidi ya Mamelodi Sundowns dakika ya 57 likakataliwa na teknolojia kwa kile kilichoelezwa kuwa mpira haukuvuka mstari asilimia 100.
Ipo wazi kuwa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali mkondo wa pili mchezo uliochezwa Afrika Kusini, Yanga ilipata bao lililozua utata kwa VAR kulikataa nchini Afrika Kusini na baada ya dakika 90 ubao ulisoma Mamelodi Sundowns 0-0 Yanga.
Kwenye changamoto za penalti Yanga ilikwama kupenya kwenye hatua ya nusu fainali kwa kufungashiwa virago kwenye mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho ndani ya dakika 90.
Ni penalti 3 walipata Mamelodi Sundowns inayonolewa na Kocha Mkuu Rhulani Mokwena ambaye aliweka wazi kuwa walikuwa na mchezo mgumu dhidi ya Yanga iliyopata penalti 2 katika kusaka mshindi wa jumla atakayetinga hatua ya nusu fainali.
MSIKIE GAMONDI
Miguel Gamondi Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kwa sasa hesabu zao ni kupata matokeo kwenye mechi zinazofuata wanatambua kila kitu kitakuwa sawa na wataendelea kupata matokeo mazuri kwenye mechi zao za ushindani.
“Tulikuwa na mchezo mzuri kwenye robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi na tulifunga bao la wazi kabisa likakataliwa kwa kilichotokea kila mmoja ameona na sasa tunaendelea kuangalia yale yanayofuata kwenye mechi zetu za ushindani.
“Pongezi kwa wachezaji kwa kuwa walifanya kazi kubwa ndani ya uwanja na mwisho kilichotokea kimetokea hakuna anayepaswa kulaumiwa kutokana na kazi iliyokuwa inafanyika uwanjani. Matokeo hayawezi kubadilika isipokuwa ni kuangalia namna nyingine yakuwa bora,”.
HUYU HAPA AZIZ KI

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz KI amebainisha kuwa malengo yao makubwa ilikuwa ni kutinga hatua ya nusu fainali kushindwa kupata ushindi kwenye penalti iliwaumiza wachezaji na benchi la ufundi.
“Tulikuwa tunahitaji kupata matokeo mazuri kwenye mechi zetu zote mbili nyumbani na ugenini, kushindwa kupata ushindi hili limetuumiza lakini bado tunamuda wakufanyia kazi makosa kwa ajili ya wakati unaofuata.
“Mashabiki wanapenda matokeo mazuri na sisi tunapenda kuona tunafikia malengo yetu. Kwa hapa kuna kitu tumejifunza hivyo tuna muda mwingine wa kurejea uwanjani na kufanya kazi kubwa katika kutafuta ushindi,”
KARIAKOO DABI HII HAPA
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imetangaza rasmi siku ya mchezo wa Kariakoo Dabi utakaowakutanisha mabingwa watetezi Yanga na Simba ambapo mchezo huo unaosubiriwa kwa shauku kubwa unatarajiwa kupigwa Aprili 20 2024 Uwanja wa Mkapa saa 11:00 jioni.
Taarifa hiyo imetolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB, Aprili 7 imeeleza namna hii “Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeupangia tarehe mchezo namba 180 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2023\2024 kati ya Yanga na Simba maarufu kama ‘Kariakoo Derby’.
“Mchezo huo ambao haukupangiwa tarehe kwenye ratiba ilioyofanyiwa marekebisho na kutangazwa Februari 2024, sasa utachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Aprili 20, 2024 saa 11:00 jioni.
“Klabu za Yanga na Simba na wadau wengine wa Ligi Kuu wamepatiwa taarifa zote kuhusu mchezo huo na maandalizi yake yanaanza mara moja ili kuhakikisha unafanyika katika kiwango cha juu kinachoendana na hadhi ya michezo mkubwa ya Ligi sita kwa ubora barani Afrika.
“Bodi ya Ligi inawatakia maandalizi mema ya wadau wote wa mchezo.”
MNYAMA KUMBUKA ALIPASUKA

Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa Mnyama Simba alipasuka kwa kupoteza pointi tatu mazima na kufungwa ndani ya daika 90 za mchezo.
Ilikuwa ni Novemba 5, 2024 raundi ya kwanza msimu wa 2023\24 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 1-5 Yanga ikiwa ni kichapo kikubwa kupokea kwa Simba zama za Roberto Oliveira.
Bao la Simba kwenye mchezo huo lilifungwa na mkandaji Kibu Dennis dakika ya 9 huku lile la ufunguzi la Yanga lilifungwa na Kennedy Musonda mapema kabisa dakika ya 3 akitumia pasi ya Yao.
