- Ligi Kuu Bara Juni 22 mzunguko wa 30, msimu wa 2024/25 itakuwa ni Juni 22 2025, Jumapili kwenye msako wa pointi tatu muhimu.
- Matokeo ya mzunguko wa 28 kulikuwa na 5G kwa timu ambazo zipo ndani ya tatu bora kwenye msimamo wa ligi.
- Ubingwa wa ligi bado kidogo Yanga SC vs Simba SC kwenye mvutano mkubwa, Kariakoo Dabi Juni 25 2025 italeta majibu mengi.
Ligi Kuu Tanzania Bara Juni 22 ni mzunguko wa 30 msimu wa 2024/25. Mechi zote 8 zitachezwa saa 10:00 kwa wababe kukutana uwanjani kusaka pointi tatu muhimu. Ikumbukwe kwamba vita ya ubingwa haijafika mwisho, Yanga SC vs Simba SC wapo kwenye mvutano. Yanga SC wanaongoza wakiwa na pointi 76 na Simba SC ina pointi 75 ikiwa nafasi ya pili.
Juni 25 2025 wababe hawa wawili Yanga SC na Simba SC wanatarajiwa kukutana Uwanja wa Mkapa saa 11:00 jioni. Hapa kuna ratiba ya mechi za mzunguko wa pili Juni 22 kwenye msako wa pointi tatu muhimu katika kukamilisha mzunguko wa pili namna hii:-
Pamba SC vs KMC FC itachezwa Uwanja wa CCM Kirumba

Mchezo uliopita Juni 18 2025 Pamba Jiji ilikomba pointi tatu dhidi ya JKT Tanzania. Katika mchezo huo wa mzunguko wa pili, bao la ushindi lilifungwa na Zabona Mayombwa ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo. Inakutana na KMC ambayo ilicheza Juni 18 2025 dhidi ya Mashujaa, ubao wa Uwanja wa Lake Tanganyika ukasoma Mashujaa 1-1 KMC hivyo wababe hawa wawili waligawana pointi mojamoja ndani ya dakika 90.
Kwenye msimamo Pamba Jiji ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 33 inakutana na KMC FC iliyo nafasi ya 10 ikiwa na jumla ya pointi 34. Pamba Jiji safu yake ya ushambuliaji ni mabao 21 imetupia huku ile ya KMC FC ikiwa imetupia mabao 25.
Simba SC vs Kagera Sugar Uwanja wa KMC Complex.

Soma hii: KenGold FC 0-5 Simba SC: magoli yote, uchambuzi, mnara umesoma 5G Tabora
Wababe hawa wanatarajiwa kukutana Uwanja wa KMC Complex. Kwenye mzunguko wa kwanza, Uwanja wa Kaitaba baada ya dakika 90 ubao ulisoma Kagera Sugar 2-5 Simba SC, pointi tatu zilikuwa mali ya Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Mchezo uliopita Juni 18 2025, ubao wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulisoma KenGold 0-5 Simba SC. Mabao ya Simba SC yalifungwa na Kibu Dennis alitupia mabao mawili dakika ya 20, 25, Ellie Mpanzu alipachika bao moja dakika ya 22, Leonel Ateba dakika ya 36 alipachika bao la nne na Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC alipachika bao la tano dakika ya 75.
Kagera Sugar walitoshana nguvu dhidi ya Namungo FC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Majaliwa kwa ubao kusoma Namungo FC 0-0 Kagera Sugar. Nafasi ya pili kwenye msimamo ipo Simba SC ikiwa na pointi 75 baada ya mechi 28. Inakutana na Kagera Sugar iliyo nafasi ya 15.
Kagera Sugar baada ya mechi 29 kibindoni ina pointi 23. Msimu wa 2025/26 itashiriki Championship kwa kuwa imeshuka daraja kama ilivyo kwa KenGold yenye pointi 16 baada ya kucheza mechi 29 msimu wa 2024/25.
Namungo FC vs KenGold, Uwanja wa Majaliwa.

Namungo FC ipo nafasi ya 12 baada ya mechi 29 ikiwa na pointi 32. Inakutana na KenGold ambayo inaburuza mkia. Safu ya ulinzi ya KenGold imeruhusu jumla ya mabao 57 ikiwa ni timu namba moja kwa kufungwa mabao mengi inafuatiwa na Fountain Gate ambayo imeruhusu mabao 55 yakufungwa.
Singida Black Stars vs Tanzania Prisons, Uwanja wa Liti.
Singida Black Stars imetoka kuvuna pointi tatu dhidi ya Dodoma Jiji. Mchezo huo ulichezwa Juni 18 2025 na ubao ulisoma Dodoma Jiji 1-2 Singida Black Stars. Kwenye msimamo Singida Black Stars ipo nafasi ya nne inakwenda kukutana na Tanzania Prisons ambayo imetoka kupoteza kwa kufungwa mabao 5-0 dhidi ya Yanga SC.
Yanga SC vs Dodoma Jiji, Uwanja wa New Amaan.

Yanga SC baada ya kuvuna pointi tatu dhidi ya Tanzania Prisons Juni 18 2025 kituo kinachofuata ni dhidi ya Dodoma Jiji, Juni 22 ikiwa ni raundi ya 30. Ikumbukwe kwamba baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Sokoine ulisoma Tanzania Prisons 0-5 Yanga SC na mabao ya Yanga SC yalifungwa na Mudathir Yahya dakika ya 31, Clatous Chama dakika ya 35, Pacome Zouzoua mabao mawili dakika ya 56 na 76. Israel Mwenda alipachika bao la nne dakika ya 60 ya mchezo.
Dodoma Jiji ipo nafasi ya 9 kwenye msimamo ikiwa imekusanya pointi 34 baada yakucheza mechi 29 inakutana na Yanga SC iliyo nafasi ya kwanza na pointi 76 baada yakucheza mechi 76 ndani ya ligi. Safu ya ushambuliaji ya Yanga SC imefunga jumla ya mabao 76 huku ile ya Dodoma Jiji ikifunga mabao 31.
Coastal Union vs Tabora United, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
Coastal Union iliyo nafasi ya 8 kwenye msimamo na pointi 34 baada ya mechi 29 itakutana na Tabora United. Tabora United ilipoteza kwa kufungwa mabao 5-0 dhidi ya Azam FC ipo nafasi ya 5 ikiwa na pointi 37 inakutana na Coastal Union ambayo imetoka kupata ushindi wa bao 1-0 Fountain Gate.
Fountain Gate vs Azam FC, Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa
Kete ya maamuzi kwa Fountain Gate ambayo haijawa na mwendo mzuri mzunguko wa pili. Pointi zake ni 29 kibindoni baada ya mechi 29 wastani wa kukusanya pointi moja kwenye kila mchezo. Inakutana na Azam FC iliyotoka kuvuna pointi tatu kwa ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Tabora United, Uwanja wa Azam Complex.
Mechi zote kupigwa saa 10:00 jioni, kiporo cha Yanga SC vs Simba SC itakuwa Juni 25 2025, Uwanja wa Mkapa na zitarushwa mubashara na Azam TV. Huu ni mzunguko wa mwisho ndani ya msimu wa 2024/25 ambao unakaribia kugota mwisho.

