KenGold FC --- Simba SCKenGold FC --- Simba SC
  • KenGold FC 0-5 Simba SC, Mnara wa 5G umesoma huko Tabora mara baada ya Mnyama kuwachakaza KenGold FC.
  • Kibu Denis ameandika rekodi ya kufunga mabao manne katika mechi nne alizocheza kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
  • Matokeo hayo yanawafanya Simba kufikisha alama 75 baada ya kucheza mechi 28 wakiendelea kusalia nafasi ya pili.

Mnara umesoma 5G huko Tabora mara baada ya Mnyama kuwachakaza KenGold FC, dakika 90 zimemalizika kibabe na ubao wa matokeo umeonyesha KenGold FC 0-5 Simba SC kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

KenGold FC 0-5 Simba SC, mchezo ulikuwaje?

Simba waliuanza mchezo huo kwa kasi na kutengeneza mashambulizi ya hatari mbele ya lango la KenGold, ambapo dakika ya 20 jitihada hizo zilizaa matunda baada ya straika wao, Kibu Denis kuipatia bao la kwanza dakika ya 20 kwa shuti kali nje ya 18.

Kibu aliipatia Simba bao hilo baada ya kuwazidi ujanja walinzi wa Kengold. Mara baada ya bao hilo Simba waliendelea kulisakama lango la KenGold na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 22 kwa shuti kali nje ya 18 kupitia kwa, Ellie Mpanzu.

Dakika ya 25, Kibu aliipatia Simba bao la tatu kwa shuti kali akiwa ndani ya 18 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Jean Charles Ahoua. Simba hawakuishia hapo kwani, Leonel Ateba aliipatia bao la nne dakika ya 36 baada ya kumalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Mpanzu.

Ahoua aliipatia Simba bao la tano dakika 75, baada ya kumalizia pasi safi iliyopigwa na Ateba akiwa nje kidogo ya 18. Matokeo hayo yanawafanya Simba kufikisha alama 75 baada ya kucheza mechi 28 wakiendelea kusalia nafasi ya pili.

SOMA HII PIA: KenGold FC vs Simba SC ‘live’: H2H, vikosi, moto utawaka, Simba watoa tamko zito leo

Vikosi vilivyoanza mchezo wa leo

Kikosi cha KenGold:

Lonje, Gabriel, Makhenzi, Kazila, Yondani (Robert 82′), Lipangile, Lukindo (Kayanda 65′), Chirwa (Mpuka 54′) Manyinyi, Morrison Ambukege

Kikosi cha Simba

Camara, Kapombe (Duchu 61′), Zimbwe Jr, Chamou (Nouma 61′), Che Malone, Kagoma (Okajepha 45′), Kibu (Mukwala 78′) Deborah, Ateba, Ahoua, Mpanzu (Mutale 61′)

Mnyama avuna pointi 6, mabao 7 kwa KenGold

Ushindi huu unaifanya Simba kujizolea pointi zote sita kutoka kwa KenGold msimu huu, ambapo kabla ya mchezo wa leo Simba walikuwa na kumbukumbu nzuri ya kuwatandika KenGold mabao 2-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza.

Huu ni mchezo wa mzunguko wa 28 wa Ligi Kuu Bara kwa Simba SC lakini unakuwa mchezo wa mzunguko wa 29, kwa KenGold FC ambao wanauendea mchezo huu wakiwa hawana cha kupoteza mara baada ya hesabu zao kuinyesha kuwa tayari wameshuka daraja.

Utofauti wa pointi hiyo moja kati ya Simba na watani zao Yanga ndio ambao umezidi kuchochea vita ya ubingwa msimu huu, ambapo mpaka sasa kama timu zote zikishinda michezo yao iliyosalia basi matokeo ya mchezo wa dabi ya Kariakoo ya Juni 25, mwaka huu yataamua bingwa.

SOMA HII HAPA: Simba SC kwenye mtihani mzito kuwakabili KenGold Juni 18 2025/ Matatizo yapo hapa

Yanga nao wasimamisha Mnara wa 5G Mbeya

Simba SC wakiicharaza KenGold Tabora, huku  watani zao wa jadi Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa mashindano hayo, nao wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Tanzania Prisons huko jijini Mbeya.

Kibu aandika rekodi Tabora

Mara baada ya kufanikiwa kufunga mabao mawili na kuasisti mara moja kwenye mchezo wa leo, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Kibu Denis ameandika rekodi ya kufunga mabao manne katika mechi nne alizocheza kwenye Uwanja huo.

Akizungumzia mchezo huo Kibu ambaye alichaguliwa mchezaji bora wa mechi amesema: “Haukuwa mchezo rahisi, tulipambana na timu ambayo haina cha kupoteza, huku tukiwa na malengo ya kupata pointi 3 na kujiweka kwenye nafasi nzuri kupigania ubingwa.

“Binafsi nashukuru Mungu kwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huu, ukweli ni kuwa kila mtu alicheza vizuri, lakini nashukuru kwa wale ambao wameona tuzo hii nistahili, hii inanipa nguvu kupambana zaidi.”

SOMA HII PIA: Simba SC kuachana na makipa wote kuelekea 2025/26/ Air Manula, Camara, Ally Salim

Hitimisho

Mara baada ya ushindi huo Simba saa wanajiandaa kuvaana na Kagera Sugar, mchezo ambao unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam huku wakitamba kuweka mikakati ya kushinda kila mchezo ulio mbele yao.

“Tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo kwa kuwa tunatofautiana pointi moja na vinara wa msimamo Yanga na kama tunataka kushinda ubingwa ni lazima tushinde mechi zote zilizobaki,” amesema Matola, kocha msaidizi Simba.

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.