ChamaChama

  • Yanga SC haigusiki kwenye kushusha vichapo vikubwa iliwabamiza Fountain Gate nje ndani mabao 9.
  • Simba SC kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji walikosa nafasi za dhahabu zaidi ya nne kufunga.
  • Licha ya Simba SC kucheza mechi 22 ipo nafasi ya pili ikiwaacha Azam FC nafasi ya tatu kwenye msimao baada yakucheza mechi 27.

Yanga SC inawadai Simba SC watani zao wa jadi deni kubwa kwenye eneo la ushambuliaji katika mabao ya kufunga msimu wa 2024/25.

Aziz
Aziz Ki kiungo mshambuliaji wa Yanga SC 2024/25. Source: Yanga SC.

Kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika, Yanga SC kwenye idara ya ushambuliaji ni habari nyingine ikiwa ni namba moja na hata nyota aliyehusika kwa mabao mengi yupo katika kikosi cha Yanga SC.

MABAO YA YANGA SC

Ni mabao 68 safu ya ushambuliaji ya Yanga SC inayoongozwa na Prince Dube imefunga ndani ya ligi ikiwa ni timu yenye mabao mengi kwa sasa huku ikiwa namba mbili kwa timu ambazo zimefungwa mabao machache uwanjani.

Clement Mzize na Dube
Clement Mzize na Dube wahambuliaji wa Yanga SC. Source: Yanga.

Baada ya kucheza jumla ya mechi 26 ambazo ni dakika 2,340 safu ya ushambuliaji ya Yanga SC imetupia mabao 68 ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 34 kwenye mechi za ushindani ndani ya ligi.

Ikumbukwe kwamba ni timu namba moja ambayo imepata ushindi mkubwa kwenye mechi zake ikipata ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya KMC na iliwatungua mabao 6-1 Ken Gold kwenye mechi za ligi zote zilichezwa Uwanja wa KMC, Complex.

Wakati ikiwa namba moja kwenye ligi na pointi zake 70 kibindoni, watani zao wa jadi Simba wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa namba mbili kwa timu yenye mabao mengi ikiwa imetupia mabao 52 baada ya kucheza mechi 22 na pointi zao ni 57.

Katika dakika 1,980 ilizocheza imekuwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 38 ndani ya uwanja. Mkali wakutupia ndani ya kikosi cha Simba SC ni kiungo mshambuliaji Jean Ahoua mwenye mabao 12 ndani ya ligi.

DENI LA SIMBA SC KWA YANGA SC

Deni ambalo Simba SC inalo kwa Yanga SC kwenye eneo la kutupia ni mabao 16 ambayo ni tofauti yao kwa sasa ndani ya ligi. Licha ya Simba SC kucheza mechi 22 ikisaliwa na mechi nne kufikia idadi ya mechi 26 sawa na Yanga SC bado safu ya ushambuliaji haijawa makini kwenye kumalizia nafasi wanazotengeneza.

Ahoua akiifungia Simba bao la -
Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC mwenye mabao 12 ndani ya ligi. Source: Simba SC.

Hilo liliwekwa wazi na Kocha Mkuu wa Simba SC Fadlu Davids ambaye alisema kuwa wachezaji wanatengeneza nafasi nyingi kwenye mechi za ushindani lakini wanashindwa kuzitumia jambo ambalo wanalifanyia kazi.

“Kwenye mechi zetu ambazo tunacheza tunatengeneza nafasi nyingi ila imekuwa ngumu kuzibadili kuwa bao, hilo tunalifanyia kazi tunaamini kwamba tutakuwa imara kwenye mechi zijazo.”

Mchezo wa kwanza ambao Simba ilipata ushindi mkubwa ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar walipopata ushindi wa mabao 5-2 llikuwa Uwanja wa Kaitaba ikiandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kupata ushindi mkubwa ndani ya msimu wa 2024/25.

Machi 14 2025, Simba ilipata ushindi mkubwa wa pili baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 6-0 Dodoma Jiji, kwenye mchezo huu nyota Jean Ahoua alikosa nafasi mbili za wazi na Kibu Dennis alifungua akaunti yake ya mabao ndani ya ligi.

Kibu Prosper
Kibu kiungo mshambuliaji wa Simba SC mwenye mabao mawili ndani ya ligi. Source: Simba SC.

Kibu kwenye mchezo huu alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo ikiwa ni tuzo yake ya kwanza ndani ya msimu wa 2024/25 na alibainisha kuwa kwake ni furaha kuona timu inashinda nay eye anatwaa tuzo ya mchezaji bora.

“Ni furaha kuona timu inashinda na kutwaa tuzo ya mchezaji bora. Kikubwa ni kuona tunapata matokeo hili ni jambo la msingi, mashabiki wazidi kuwa nasi kwenye mechi zetu zote.”

MKALI WA MABAO HUYU HAPA

Mkali wa mabao ndani ya ligi ni Clement Mzize ambaye yupo ndani ya kikosi cha Yanga SC kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi akiwa kafunga jumla ya mabao 13 msimu wa 2024/25.

Kwenye mchezo uliopita Aprili 21 dhidi ya Fountain Gate Mzize alifunga mabao mawili na alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo baada ya dakika 90 wakati wakisepa na pointi tatu mazima uwanjani.

MKALI KWENYE KUHUSIKA NA MABAO MENGI

Prince Dube nyota wa Yanga SC ni mkali kwa mastaa waliohusika kwenye mabao mengi akiwa nayo 20 ambapo kafunga mabao 12 na katoa pasi 8 akiwa ni namba moja kwa mastaa waliohusika kwenye mabao mengi ndani ya ligi.

Ikumbukwe kwamb Dube ni nyota wa kwanza kufunga hat trick kwenye ligi alifungua ukurasa kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa uliochezwa Uwanja wa KMC Complex.

Share this: