KISHINDO-SaidoSaido
Inonga
Inonga beki wa Simba ambaye anatajwa kuwa huenda hatakuwa sehemu ya kikosi msimu wa 2024/25. Source: Simba

KISHINDO kikubwa kinakuja kwa Simba kutokana na mpango kazi wa kuboresha kikosi hicho kwa msimu wa 2024/25 ili kurejea kwenye ubora kwenye mechi za ushindani za kitaifa na kimataifa ndani ya uwanja.

Ipo wazi kuwa Simba imegotea nafasi ya tatu msimu wa 2023/24 ikiwa na pointi 69 kibindoni haikuwa na mwendo mzuri kwenye mechi zake jambo ambalo liliongeza huzuni kwa viongozi na mashabiki wa timu hiyo.

Kutoka kwa benchi la ufundi imewekwa wazi kuwa kuna maboresho makubwa yanakuja hivyo timu mpya inasukwa kwa ajili ya kurejea kwenye ushindani kwenye anga la kitaifa na kimataifa.

 

Ni Juma Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba alibeba mikoba ya Abdelhak Benchikha aliyebwaga manyanga na mchezo wake wa mwisho kabla ya kusepa ndani ya Simba Benchikha kukaa benchi alishuhudia ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Yanga 2-1 Simba.

 

Mgunda amekaa benchi kwenye mechi tisa akiambulia ushindi kwenye mechi 7 na sare mbili zote ilikuwa ugenini, Namungo 2-2 Simba ulikuwa mchezo wa kwanza kuongoza akishuhudia Willy Onana akifunga bao la uongozi na Kagera Sugar 1-1 Simba ilikuwa sare yake ya pili, Uwanja wa Kaitaba walipogawana pointi mojamoja.

 

Funga kazi ilikuwa ni Mei 28 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 2-0 JKT Tanzania huku nyota Onana akifunga bao la pili kwenye mchezo huo ikiwa ni funga kazi mazima 2023/24 na Simba ikigotea nafasi ya tatu huku mabingwa wakiwa ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa.

 

Mgunda amesema: “Nimeongoza timu kwenye mechi 9 kuna masuala ya kiufundi ambayo yatafanyika hasa maboresho kwa wakati ujao. Tunatambua kwamba ili timu ifanye vizuri lazima kuwe na maboresho hivyo Simba mpya inakuja.

 

“Huwezi kukwepa kuhusu maingizo mapya kwenye timu hilo lipo. Mashabiki watulie wawe na subira kwa kuwa kila timu ilikuwa na malengo yao mwisho kila kitu kimekuwa kama ambavyo kimetokea, tulikuwa tunapenda kumaliza nafasi ya pili lakini tumekwama ni sehemu ya matokeo.”

MATAJI ILIYOPISHANA NAYO

Ipo wazi kuwa kwa msimu wa 2023/24 Simba imepishana na mataji yote muhimu iliyokuwa inahitaji kutwaa mwanzo wa msimu mpya wa ligi. Baada ya ligi kugota mwisho haikuwa hivyo kama awali.

Imepishana na taji la ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika na ni shuhuda bingwa mpya wa CRDB Federation Cup akitangazwa ambaye ni Yanga mbele ya Azam FC kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika iligotea hatua ya robo fainali lakini kwa msimu ujao itakuwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kugotea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.

HUYU HAPA SEMAJI WA SIMBA

AHMED
AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba. :Source Simba.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa nyakati ambazo wamepitia ni ngumu na hazijawafurahisha hivyo wanapambana kurejea kwenye ubora.

“Hatujapenda na tumekuwa na huzuni kwa kuwa tumepoteza kila kitu ambacho tulikuwa tunakipigania kwenye msimu ulioisha.

“Yote kwa yote yaliyopita tunayachukua na tunakwenda kuyafanyia kazi kwa ajili ya kuwa bora wakati ujao mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.”

REKODI YAO

Saido
Saido Ntibanzokiza kiungo wa Simba. Source: Simba.

Simba inaingia kwenye timu yenye rekodi ya kuwa timu ambayo imefunga bao kwenye kila mchezo ndani ya ligi msimu wa 2023/24 licha ya kugotea ikiwa nafasi ya tatu.

Katika mechi 30 ambazo ilicheza timu hiyo safu yake ya ushambuliaji ilifunga jumla ya mabao 59 ikiwa ni namba tatu pia kwa timu ambazo zimefunga mabao mengi kwenye ligi.

Namba moja ni Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ambayo ilimaliza msimu ikiwa na mabao 71 kinara wa utupiaji akiwa ni Aziz KI aliyefunga jumla ya mabao 21 ndani ya ligi.

Ki ni mkali wa mguu wa kushoto ambapo alitumia mguu huo kufunga mabao 17 na mabao matatu alifunga kwa kutumia mguu wa kulia na bao moja alifunga kwa pigo la kichwa ilikuwa dhidi ya Tabora United mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Kwa upande wa Simba namba moja kwa utupiaji ni Saido Ntibanzokiza ambaye alifunga mabao 11 msimu wa 2023/24 ndani ya ligi na inaelezwa kuwa nyota huyo huenda akasepa ndani ya kikosi hicho.

Share this: